Monday, 24 June 2019

CHADEMA YAMVUA UANACHAMA DKT. MAKONGORO MAHANGA

Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) kimemvua uanachama Dk. Makongoro Mahanga baada ya kubainika anakihujumu chama hicho pamoja na kutoa siri za chama kuzipeleka CCM.
Mwenyekiti wa Chadema tawi la Migombani jimbo la Segerea, Baraka Mwalukunga, alisema wamegundua ni msaliti ndani ya chama na kuamua kumvua uanachama.

Alisema waliweka kikao cha mwenendo wa nidhamu cha kumjadili Dk. Mahanga baada ya kuitwa katika vikao mbalimbali ili kutoa utetezi juu ya tuhuma anazomkabili ama kujieleza jinsi anavyofanya makosa ndani ya chama.

“Amekuwa akikaidi, kudharau vikao vya chama hivyo kutokana na mwenendo wake wa usaliti na kufanya mapinduzi ndani ya chama kwa mujibu wa katiba ya chama ibara ya 5 (4) kifungu cha tatu natangaza kumvua uanachama tangu Juni 21 mwaka huu,” alisema

Aliongezea kuwa:”Kwa mamlaka hiyo Dk. Mahanga sio mwanachama wa Chadema tumechoka na usaliti wake,”

Dkt. Makongoro Mahanga

Alisema Makongoro Mahanga amekuwa akikiuka katiba kanuni na kosa kubwa ni usaliti na amekuwa akitoa siri za chama na kuzipeleka CCM na ushahidi wanao kwani vikao hivyo alikuwa akivifanya nyumbani kwake.

Aidha, Mwalukungu alisema Mahanga amekuwa akisababisha migogoro kwa namna anavyotaka yeye na kuwaondoa wanachama bila kufuata utaratibu.

Alisema wamemuita ili aweze kutoa utetezi lakini amekuwa ni mkaidi na kudharau mamlaka ya chama.

Alisema Mahanga alikuwa akifanya mambo mbalimbali ya kukihujumu chama na kujikuta wakitumia nguvu kubwa ya kupambana wakati taarifa hizo anazifanya akiwa nyumbani kwake.

“Usaliti ni kosa kubwa kuliko mengine tawi limeridhia kumuondoa kitendo cha kukataa kutii ngazi ya tawi hawezi kuendelea kuwa mwanachama,” alisema.

Mkongora Mhanga alishawahi kuwa Mbunge wa Ukonga kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 ambapo jimbo hilo liligawanyika na kuzaliwa jimbo la Segerea ambapo aliongoza katika kipindi cha miaka mitano.

Mahanga alishawahi kuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira na baada ya hapo alihama chama cha CCM na kuhamia Chadema ambapo alikuwa ni Mwenyekiti wa chama (Chadema) mkoa wa Ilala.
               

No comments:

Post a Comment